Mtandao wa mashirika yanayopinga ndoa za utotoni Tanzania umesikitishwa na msimamo wa serikali kuhusu kutokuwa tayari kubadilisha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwenye vipengele vinavyoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa mika 14 au 15. Msimamo huo wa serikali ulitolewa na Waziri wa Katiba na Sheria,Prof. Palamagamba Kabudi mnamo tarehe 19 April 2018 bungeni, akijibu maswali yaliyohusiana na mabadiliko ya sheria, ikiwemo sheria ya ndoa na umri wa mtoto wa kike kuolewa.
Nukuu
‘’..........baada ya (serikali) kutafakari kwa umakini suala la mabadiliko ya sheria ya ndoa linahitaji umakini mkubwa sana......sheria hii ya ndoa ya 1971 ukiifumua leo kuipitisha ndugu zangu ni ngumu.......sheria yoyote iliyofikiwa kwa maafikiano inahitaji umakini katika kuibadilisha....sheria hii ya ndoa ya 1971 ni sheria iliyoendelea sana ukilinganisha na mataifa mengine lakini hiyo haina maana tusiangalie mapungufu...tukieendea kwa haraka tutavuruga zaidi kuliko kujenga....kwa hio tujenge muafaka wa taratibu.....ni kweli kabisa serikali imekata rufaa kuhusu umri wa mtoto kuolewa lakini (serikali)tunapokata rufaa hatuangalii hoja tunaangalia matokeo.....’’- Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria
Ikumbukwe kuwa Julai 2016 Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa maamuzi kwamba vifungu vya 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike wa umri wa miaka 14 au 15 kuolewa ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 katika kesi ya Rebeca Gyumi dhidi ya mwanasheria mkuu wa serikali. Mahakamu Kuu iliitaka serikali kufanya maboresho ya vifungu hivyo ili umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 kwa Jinsi zote. Katika kutekeleza hilo, Septemba 2016 serikali ilitoa ahadi ya kuanza mchakato wa kubadili Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971. Cha kushangaza badala yake serikali ilikata rufaa na kufungua kesi Mahakama ya Rufani kesi namba 204/2017 kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa.
1
Katika muendelezo wa azma hio ya serikali, mnamo tarehe 19 April 2018, Mtandao umeshuhudia serikali ikishikilia msimamo wake wa kusita kubadili vifungu hivyo katika sheria ya ndoa 1971. Waziri wa Katiba na Sheria, Mh. Waziri, Prof. Kabudi, alieleza kwa ustadi mkubwa sababu ya wasiwasi wa serikali wa kubadili sheria ya ndoa licha ya ahadi iliyotolewa na serikali 2016. Katika maelezo ya waziri, hoja kuu sita zilijitokeza ambazo alitumia kuliaminisha Bunge la Jamhuri ya Munngano wa Tanzania na watanzania kwa nini si muda muafaka kubadili sheria ya ndoa kwa sasa. Hoja hizi ni kama zifuatazo;
1. Ndoa za utotoni huwakinga watoto wa kike kutokuwa na mahusiano ya kingono nje ya ndoa na kuwasaidia wasizae wakiwa majumbani;
2. Ndoa za utotoni ni mkakati wa makusudi wa serikali katika kumlinda mtoto kutokana na mimba nje ya ndoa ambazo zinaweza kuleta fedhea kwa binti na familia yake (Positive Discrimination);
3. Licha ya mapungufu kadhaa, sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni moja ya sheria bora kabisa duniani;
4. Tunahitaji maridhiano ya kitaifa kabla ya kubadili sheria ya ndoa;
5. Suala la Imani za kidini na mila kuwa hoja ya kuendelea kuruhusu umri wa
mtoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18;
6. Katika kubadilisha sheria ya ndoa serikali haiangalii hoja bali inaangalia
matokeo ya mabadiliko ya sheria hiyo.
Baada ya kuzisikiliza na kuzichambua kwa umakini hoja za serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, Mtandao umekubaliana na baadhi ya hoja na vilevile kutokukubaliana na baadhi ya hoja.
2. Mambo Tunayokubaliana
Mtandao unakubalina na hoja zifuatazo:
i. Ni kweli kabisa, suala la ndoa linagusa maisha ya watu/jamii, ikiwemo masuala ya mila, tamaduni na imani za watanzania;
ii. Ni kweli kabisa kwamba masuala ya mila na imani za watu yanahitaji maridhiano na ni vema kuyaendea kwa uangalifu mkubwa;
iii. Ni kweli kabisa kwa muktadha na mazingira yaliyokuwa mwaka 1971, ilikuwa ni sahihi sheria ya ndoa kutungwa kwa jinsi ilivyo sasa;
iv. Ni kweli kabisa kwamba sheria ya ndoa ilipatikana kwa muafaka wa kitaifa (compromise) ;
v. Ni kweli kabisa tunahitaji muafaka wa kitaifa kwenye kujadili masuala yanayohusu ndoa;
3. Mambo Tusiyokubaliana
2
i. Si sahihi kuhusianisha ndoa za utotoni na dini/mila. Kama tutakavyofafanua kwenye hoja zilizotolewa na Mh. Waziri, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ndoa za utotoni na dini;
ii. Ndoa za utotoni haziwezi kuwa mpango wa kumlinda mtoto wa kike (Affirmative action) kwani madhara yake ni makubwa zaidi kwa binti, familia na nchi kwa ujumla;
iii. Si kweli kwamba serikali kwa kubadilisha kifungu cha 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya 1971 kutahitaji kufumuliwa kwa sheria hio;
iv. Sio sahihi kwa serikali kutetea mila, tamaduni au imani za kidini zinazomkandamiza mtoto wa kike kwa kigezo kwamba inagusa maisha ya watu kwa kufanya hivi serikali inaridhia kugandamiza kundi Fulani kwa maslahi ya wengi;
v. Sio sahihi serikali kuendelea kuchukua muda mrefu kutafakari suala ambalo linaathiri sehemu kubwa ya watu wake, ni muda muafaka kwa serikali kuchukua hatua na kuweka bayana utaratibu wa kujenga maridhiano ya kitaifa juu ya umri wa mtoto wa kike kuolewa.
4. Ufafanuzi wa Hoja Za Msingi Kwenye Maelezo Ya Waziri
Mtandao umezifafanua hoja za serikali kama ifuatavyo:
I. Ndoa za utotoni huwakinga watoto wa kike kutokuwa na mahusiano ya kingono kabla ya ndoa
Mtandao unapingana na misingi ya hoja hii kwa kile inachokiona kwamba kujihusisha na vitendo vya ngono kabla ya ndoa ni ukosefu wa maadili sio kwa mtoto wala mtu mzima. Vilevile kama lengo ni kudhibiti mahusiano kabla ya ndoa basi kwa nini anayelazimika kuingia kwenye ndoa kabla ya kuwa mtu mzima ni mtoto wa kike peke yake? Hoja ya msingi ni umri wa mtoto na sio suala la ngono kabla ama baada ya ndoa.
Kwa kuzingatia, Maslahi mapana ya mtoto (Best interest of the child) kama yalivyoelezwa na Sheria ya Mtoto ya 2009 na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia, si sawa watoto kuingizwa kwenye ndoa kabla ya kuwa watu wazima. Pia kupitia Sheria ya Kanuni ya Makosa Adhabu, Sura Namba 16, na Kupitia Sheria ya Elimu, ni kosa la jinai kuwa na mahusiano ya kingono na mtoto au mwanafunzi. Lengo la sheria hizi ni kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ngono wakati sheria ya ndoa inahalalisha mtoto wa kike kuolewa kabisa.
Kuwaozesha watoto wa kike kabla ya kuwa watu wazima kwa kisingizio cha kuwalinda na mahusiano ya kingono kabla ya ndoa si dawa ya tatizo hilo. Suala la watoto kuwa na mahusiano kabla ya ndoa ni matokeo ya udhaifu wa malezi na mmomonyoko wa maadaili katika jamii. Kama kweli tuna nia ya dhati ya kupunguza mahusiano ya kingono kwa watoto ni vyema tukajielekeza katika
3
kurudisha na kusimamia maadili yetu na sio kwa kuwaingiza kwenye ndoa za utotoni watoto wa kike.
II. Ndoa za utotoni ni mkakati wa makusudi wa serikali katika kumlinda mtoto wa kike kutokana na mimba nje ya ndoa ambazo zinaweza kuleta fedheha kwa binti na familia yake (Positive Discrimination)
Hoja ya pili, katika maelezo ya Mh. Waziri ni kwamba serikali inaona kuwa ndoa za utotoni ni sehemu ya mkakati wa makusudi katika kumlinda mtoto wa kike kuepukana na mimba nje ya ndoa kwa kuweka umri tofauti kati ya mtoto wa kike na wa kiume wa kuoa na kuolewa. Utofauti huo, Mh. Waziri anasema ni “ubaguzi chanya’’ (positive discrimination) au hatua za makusudi (affirmative action). Katika hoja hii kuna upotoshaji juu ya dhana ya hatua za makusudi na ni katika mazingira gani hatua hizo zitatafsiriwa kama hatua za makusudi na sio ubaguzi chini ya Ibara ya 13(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimsingi, dhana ya hatua za makusudi au ubaguzi chanya, kama ilivyotumika kwenye Katiba na kwa kuangalia historia namna ambavyo imekuwa ikitumiwa katika nchi mbalimbali, hulenga kuchukuliwa ubaguzi chanya au hatua za upendeleo maalumu kwa kundi moja, au baadhi ya watu dhidi ya wengine, kwa lengo la kuliinua kundi hilo/watu hao kuondokana na sababu za kihistoria ambazo zimelifanya kundi hilo kuachwa nyuma kwenye ushiriki wa mambo fulani. Mfano mzuri wa hatua za makusudi ni uwepo wa nafasi za ubunge kwa wanawake kupitia viti maalumu kwa kuzingatia kwamba kundi la wanawake kihistoria limekuwa likibaguliwa katika nafasi za Uongozi na kusababisha ushiriki wa kundi hilo kuwa duni. Katika muktadha wa ndoa za utotoni kumuoza mtoto wa kike si ubaguzi chanya wala si hatua za makusudi bali ni kumkandamizia na kumnyima maslahi yake kama mtoto.
Utafiti wa Benki ya Dunia ikishiriana na shirika la International Centre For Research on Women 2017, “ The economic Impact of Child Marriage” unaonesha ni kwa kiasi gani nchi zinapata harasa ya kiuchumi kutokana na ndoa za utotoni. Tafiti hii inaonesha kwamba mpaka kufikia 2030, mwaka ambao, kupitia malengo endelevu ya dunia, nchi zinazoendelea zitakuwa zimepata hasara ya karibia dola za kimarekani trilioni. Ukiachia hasara hii ya kiuchumi kuna madhara mengine mengi yanayosababishwa na ndoa za utotoni ikijumuisha watoto wa kike kukosa haki ya elimu hususan watoto walioko nje ya mfumo rasmi wa elimu;kunyimwa haki ya usawa – usawa kati ya watoto wa kiume na kike; kunyimwa haki ya utu - inatweza utu wa mtoto wa kike kwa kuolewa bila ridhaa yao; kuwa katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili wa kijinsia; Matatizo ya uzazi; kubeba mimba kabla ya miili kuwa tayari kuzaa na hivyo kupelekea kupata matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua; Vifo vya wakati wa kujifungua (maternal mortality)(Kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch “vijana balehe wenye umri wa miaka 5-19 wana uwezekano wa kufariki wakati wa kujifungua mara mbili zaidi ya wanawake waliopo katika umri kati ya mika 20 na 24.” Tafiti za hivi karibuni zilizotolewa na Wizara ya Afya,
4
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonyesha kwamba hatari ya vifo vya kinamama kutokana na ndoa za utotoni ni 32%), na kuishia kwenye wimbi la umaskini baada ya kunyimwa fursa ya kupata au kuendelea na elimu.
Inawezakana kabisa, kwa mazingira ya mwaka 1971 wakati sheria ya ndoa inatungwa ilikuwa sahihi kuweka umri wa ndoa kama ambavyo umewekwa kwenye sheria kwa sababu kwa walio wengi, ukomo wa elimu ulikuwa darasa la saba. Lakini kwa sasa mazingira yamebadilika na kuna maendeleo makubwa sana yanapigwa na nchi kwenye nyanja mbalimbali. Kwanza, kama nchi kupitia Katiba tuna haki za binadamu ambazo hazikuwepo mwaka 1971; Pili, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ambayo inapinga ndoa za utotoni; Tatu, Msingi mkuu wa maslahi bora ya mtoto kupitia sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009; Nne, Sera ya elimu bure mpaka kidato cha nne na uwepo wa shule za sekondari kwenye kila kata, pamoja na uwepo wa sheria ya elimu inayokataza wanafunzi kuwa na mahusiano ya kingono pamoja na ndoa kwa wanafunzi. Mambo haya yote ni kiashiria tosha kuwa vifungu na 13 na 17 vya sheria ya ndoa vinahitaji mabadiliko.
III. Hoja kuhusu Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kuwa bora duniani
Mtandao unatambua kwamba Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ina vipengele vingi vizuri na vinapaswa kuenziwa, pia kuna maeneo ambayo kama nchi tuko mbele ukilinganisha na nchi nyingine. Licha ya ukweli huu, Mtandao haukubaliani na hoja za serikali kutumia visingizio vya mila na imani za watu kukwepa kufanya mabadiliko ya kifungu cha 13 na 17 kinachoruhusu watoto wa kike kuolewa katika umri wa miaka 14 au 15. Ikumbukwe kuwa, Tanzania kama nchi haina dini wala haifungamani na itakadi zozote za kimila licha ya kwamba inaheshimu uhuru wa Wananchi wake kuwa na mila na imani zao. Hivyo basi utungaji wa sheria unapaswa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na sio mila na imani za watu.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatamka wazi kwamba mila na desturi zinazopingana na Katiba hazina nafasi kwenye masuala ya haki za wananchi. Hivyo basi, ni wakati muafaka kwa serikali kuimarisha ulinzi kwa watoto wa kike bila kujali mila na imani kandamizi.
IV. Hoja ya maridhiano ya kitaifa kabla ya kubadili sheria ya ndoa
Mtandao unakubaliana na misingi ya hoja hii kwani mabadiliko yoyote ya kisheria yanawalenga watu hivyo ni vyema walengwa kushirikishwa. Hata hivyo, jitihada za kutetea maboresho ya sheria hii hazijaanza leo, zimeanza tangia miaka ya 1990 na katika kipindi chote hicho hakuna kundi ambalo limewahi kujitokeza hadharani kupingana na hoja ya umri wa mtoto wa kike kuolewa kuwa 18.
5
Mtandao unapenda kuikumbusha serikali na Mheshimiwa Waziri kwamba sheria yoyote inayozingatia misingi ya haki za binadamu ni lazima itakwaza mila na imani ambazo zinakinzana na haki za binadamu. Hivyo serikali isiwe mtetezi wa mila na imani kandamizi zinazopalilia mfumo dume na kutweza utu wa mwanamke. Ni wakati muafaka kwa serikali kuanzisha mijadala huru yenye lengo la kutafuta muafaka juu ya mabadiliko ya sheria ya ndoa, majadiliano yatakayoongoza na kujikita katika msingi wa maslahi bora ya mtoto (Best interest of the child).
V. Hoja kuhusu mila na Imani za kidini kuendelea kuruhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa chini ya miaka 18
Mtandao unatambua kwamba zipo mila mbali mbali kandamizi zinarohusu ndoa za utotoni lakini Mtandao unachelea kuamini kwamba zipo dini zinazoruhusu ndoa za utotoni. Katika maelezo yake Mh. Waziri anashawishi tuamini kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ndoa za utotoni na dini hasa ya Uislam. Hoja hii ni dhanishi na inapingwa na tafiti. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na REPOA na Shirika la Jukwaa la utu wa mtoto – CDF na wengineo mwaka 2017 unatanabaisha kwamba sababu kuu za ndoa za utotoni ni umaskini; kuendelezwa kwa mila na desturi kandamizi; ubaguzi wa kijinsia; na kulinda hadhi ya familia kwa lengo la kuepusha fedheha pale binti anapozalia nyumbani.Hakuna utafiti unaohusisha moja kwa moja imani za kidini na ongezeko la ndoa za utotoni.
Vilevile udhaifu wa hoja hii unathibitishwa na nchi ambazo 90% ya wakazi wake ni waislam lakini wamefanikiwa kubadili sheria ya ndoa kwa kuweka umri wa ndoa kwa mtoto wa kike na wa kiume miaka 18. Mfano wa nchi hizo kama Sri lanka, Bangladesh, Indonesia pamoja na nchi zingine zinazotuzunguka ambazo zina makabila mengi na hivyo kuwa na mila na tamaduni zinazotofautiana lakini bado zimeweza kuweka umri wa ndoa kwa mtoto wa kike na kiume kuwa ni kuanzia miaka 18 nchi hizo ni pamoja na Malawi, Rwanda, Uganda na Kenya.
VI. Kuhusu Serikali kutokuangalia hoja bali kuangalia matokeo katika kubadilisha sheria ya Ndoa 1971.
Mtandao, unaikumbusha serikali kuzingatia kwa mkazo athari anazokumbana nazo mtoto wa kike kwa kuruhusu kuolewa akiwa chini ya miaka 18 kama moja ya matokeo wanayoyazingatia katika utungaji wa sheria. Pia serikali haipaswi kujivua jukumu la ulinzi wa haki za mtoto wa kike kwa kisingizio cha mila, desturi, dini wala sababu nyingine yoyote kwani mtoto wa kike anaitegemea serikali kama mtetezi wake nambari moja.
Kwa minajili ya kutokuzingatia hoja serikali inakubali kwamba iko tayari kukandamiza maslahi bora ya mtoto wa kike kwa lengo la kulinda na kueteta mila, desturi na imani kandamizi.
6
Hivyo basi Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni Tanzania tunatoa mapendekezo yafuatayo:
1. Serikali iepuke kutetea mfumo dume, mila, desturi na imani kandamizi na badala yake ifanyie kazi kwa hoja na tafiti zinazopendekeza kubadilishwa kwa vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa 1971 kwa lengo la kulinda maslahi bora ya mtoto wa kike hapa nchini;
2. Serikali iepuke kuwa sehemu ya kulaumu mifumo kandamizi bali ichukue hatua madhubuti ikiwemo uwepo wa mijadala ya wazi ili kujenga muafaka wa kitaifa kuhusu umri wa mtoto wa kike kuolewa;
3. Serikali iache kujichanganya katika utekelezaji wa sera na mikakati yake iliyojiwekea yenyewe ikiwemo Mpango kazi wa kitaifa wa kuondoa aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto 2017 - 2022 ikiwemo kuondoa ndoa za utotoni;
4. Wadau wote ikiwemo vyombo vya habari, taasisi za dini, viongozi wa kisiasa na asasi za kiraia tuungane katika kuendelea kuielimisha jamii kuhusu ya madhara ya ndoa za utotoni na tushirikiane katika kupinga na hatimaye kutokomeza ndoa hizi ili kumpa fursa mtoto wa kike kuishi ndoto zake na kufurahia utu wake.
Tamko hili limetolewa leo tarehe 30 April 2018 na mtandao wa kutokomeza ndoa za utotoni Tanzania ambao una wanachama zaidi ya 40 kutoka mikoa mbalimbali Tanzania.
Asanteni,
Valerie Msoka
Mwenyekiti wa Mtandao - TECMN
No comments:
Post a Comment